Ukuta wa Ukimya: Uchunguzi wa awali kuhusu ukatili dhidi ya wanawake Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali ya Zanzibar imeanzisha jumuiya/vituo kadhaa muhimu vya kushughulikia Ukatili Dhidi ya Wanawake kama vile Kamati za Ukatili wa Kijinsia, Mtandao wa Polisi wanawake,Madawati ya Polisi ya kushughulikia jinsia, na hivi karibuni, kituo kinachotoa huduma nyingi mahali pamoja (Mkono kwa Mkono) katika Hospitali ya Mnazi Mmoja. Hata hivyo, kasi ya mabadiliko imekuwa taratibu na inakabiliwa na upungufu wa rasilimali. Haki, usalama, na misaada haipatikani kwa wanawake wengi walioko Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba. Uchunguzi huu unadhihirisha kwamba kushughulikia Ukatili Dhidi ya Wanawake na kuvunja “ukuta wa ukimya” unahitaji mbinu za kuzikabili/kupambana na changamoto mbili. Kwanza, maadili ya jamii na mitazamo ambayo inachukulia Ukatili Dhidi ya Wanawake kuwa ni suala la jamii na sio kosa la jinai, na kuhimiza ndoa au ulipaji wa fi dia lazima zipigwe vita kupitia programu za ufahamu wa sheria na utoaji misaada kwa waathirika wa Ukatili Dhidi ya Wanawake. Pili, taasisi na huduma za sheria lazima ziimarishwe ili ziweze kutoa njia mbadala zilizo nzuri za usuluhishi usio rasmi wa makosa ya Ukatili Dhidi ya Wanawake.